Header Ads

Header Ads

KILA MTU ANAWAZA NA KUTAMANI KUWA ‘Mr.Somebody’.

         Mwenyezi Mungu ametuumba Wanadamu wote tuwe sawa, na zaidi wote   tumwabudu yeye Muumba aliyeumba Mbingu na Ardhi.Lakini kila Mwanadamu ameumbwa na Moyo wa matamanio ya kufanikiwa kimaisha akijifunza na kupata msukumo kutoka kwa watu waliomtangulia katika Tasnia anayohudumu kwa lugha ya Kimombo wanaita“Role models”.

          Msukumo au kichocheo kikubwa kinachoweza kukusukuma kutamani siku moja nawe uwe kama fulani yaani’Mr. Somebody’ si kingine bali ni Mafanikio.Unaamua kuwaza au kubadili mawazo yako ya awali ya kuwa Daktari na kubadili”Gia” angani  ukafikiria kuwa Mwanahabari nguli kabisa.Ndiooooooooooo………..,hakuna Ndumba wala Uchawi,inawezekana!

        Nikiwa tangu ningali kijana mdogo kabisa miaka ya tisini hivi,nilikuwa na ndoto ya walau kuwa Mwandishi wa Vitabu kama siyo kuwa Mwandishi wa Habari.Namkumbuka Baba yangu mdogo anayeitwa Pembe Rajab Kizigo aliwahi kuja nyumbani kwetu kwa  Mzee Seleman Mahuruku akiwa na  Mtangazaji mmoja nguli enzi hizo wa Radio Tanzania(RTD) leo hii TBC Taifa,aliyeitwa Abisai Steven marehemu  kwa sasa.Wakati naongea na kujieleza kiukweli,Abisai Steven aliniambia naweza kuwa Mwandishi kwa siku za usoni.Kipindi hicho Marehemu Abisai Steven alikuwa amepitia Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria pale Ruvu JKT Mlandizi mkoani Pwani.

           Sikuweza kutambua nini alimaanisha kwa kuwa nilikuwa sijui lolote kwa alichokiongea.Hata nikiwa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kilangalanga,nakumbuka Mwalimu wangu wa Kiingereza aliyeitwa Mr.Komba na Walimu wa Kiswahili, Mwalimu Ngimbwa na Mwalimu Thomas Tumbo kwa nyakati tofauti waliwahi kuniambia nina kipaji kikubwa cha Uandishi lakini kiukweli sikutilia mkazo na kile walichokuwa wakinieleza.

         Nilianza na utangulizi huo kwa kujikumbusha kidogo jinsi gani mtu unaweza kutamani au kuwa mtu fulani lakini baadae ukawa mtu gani! Na hii najiona wapi nipo na wapi naelekea kuwa iwapo Mwenyezi Mungu ataendelea kunipa uhai maana bila yeye mimi si kitu.

           Acha sasa niongelee nilichotaka niandike hapa,kuna watu wanaitwa “Wachambuzi”.Kuna Wachambuzi wa masuala mbalimbali lakini hapa nataka niwaongelee Wachambuzi wa SOKA.Kama wewe ni mtu wa Soka bila shaka jina la Leaky Abdallah ‘Dokta Leaky’ si geni kwako!

Huyu ndiye kinara wa mwanzoni kabisa katika uchambuzi wa Soka hapa nchini.Uwezo wake wa uchambuzi umeweza kuwashawishi vijana wengi kama Shaffih Dauda,Eddo Kumwembe,Ezekiel Kamwaga’Mr.Liverpool,Saleh Alli,Ally Mayai,Ibrahimu Masoud Maestro na wengine weeeeeengi.Mafanikio ya Dokta Leaky,yameweza kuwavutia hao na vijana wengine wengi kujikita katika Uchambuzi wa Soka.

Mafanikio ya kizazi cha kina Shaffih Dauda na wenzake ambapo mimi namuona Shaffih Dauda kama Mchambuzi aliyefanikiwa zaidi hasa katika suala la kujiongeza,ndiyo yamechochea zaidi ongezeko la vijana wengi kujikita katika Uchambuzi.Kuna Geof Leah,Ally Kamwe,Nicasious Agwanda Suso,Mussa Mwakisu,Oscar Oscar Jr,Mussa Kawambwa,Edgar Kibwana,Tigana Lukinja,George Ambangile na wengine weeeengi ambao pengine nimeshindwa kuwaandika kwa bahati mbaya tu si lengo langu kufanya hivyo,wote hao wameweza kuvutiwa na watu hao.Pia bila  kumsahau Mwalimu Fundi wa Uchambuzi wa mpira Mwalimu Alex Kashasha ambaye huyu ameongeza tija sana ya Wachambuzi wa Soka katika suala zima la ‘Utaalamu’.

        Wewe kijana unayewaza kuwa’Mr.Somebody’ siku moja,tambua haishindikani.Kikubwa ni kujitambua unachotaka ni nini? Na  mahitaji yake ni nini? Kila Nyanja,kila sekta na kila jambo linahitaji kujipanga,kujituma na kufanya ubunifu wa hali ya juu sana ili kujiimarisha vizuri katika ushindani.Mwisho kabisa niwaambie tu vijana ama watu wanaotamani kuwa Wachambuzi wa Soka na Michezo mingine,ichukulieni kama Taaluma yaani mjiongeze katika kusomea walau hata kozi za awali ili muwe na uweledi wa kile mnachochambua.Kuna wimbi kubwa sana la watu wanaohitaji mafanikio mara tu baada ya kuona mtu fulani amefanikiwa.Amini Ndoto zako,jiongeze.
           Wasalaaam……….

           

2 comments: